Home » Articles » COMPUTER

Kwanini waliomaliza kusomea Graphic Designing hushindwa kufanyia kazi?

NI GRAPHIC DESIGNER LAKINI HUWEZI KUFANYA GRAPHIC DESIGNING

Kwanini waliomaliza kusomea Graphic Designing hushindwa kufanyia kazi?

 

Graphic Designing ni elimu inayotolewa kwa mtu kwa mafunzo ya kuchora, kuandika, kupamba, ketengeneza picha mbalimbali kwa ujuzi wa computer. Ujuzi huu hutumia msaada wa program maalum ambazo hutumika katika kufanya graphic designing.

 

Michoro yenye mapambo, matangazo, maandishi yanayovutia na picha mbalimbali unazoziona ndani na nje ya internet ni matokeo ya kazi hii ya graphic designing. Kazi hii imekuwa ni bora kwa ulimwengu wa sasa wa kiteknolojia kwani watu huhitaji sana vijana wenye ujuzi wa hii, kuwatengenezea matangazo, michoro na mambo mengi ya kuvutia katika kutangaza biashara zao.

 

Hata wale wanaotengeneza kadi za harusi au za mchango na nyinginezo hutumia ujuzi huu.

 

Kwa wale ambao ndio wanaanza kujifunza hutumia sana Microsoft Office Publisher kwani ndio program rahisi na haina mambo mengi ya kuchanganya na hata kuisomea hii katika vyuo inakuwa na gharama ndogo ukilinganisha na nyinginezo. Mara nyingi wanaotengeneza kadi mbali mbali kama vile za harusi, mualiko, mchango, vitambulisho vidogo hupenda sana kutumia Microsoft Office Publisher.

 

Kwa sasa program kubwa sana inayotumika ulimwenguni katika kufanya graphics ni Adobe Photoshop na Adobe illustrator lakini kuna tofauti sana hapo, Adobe Photoshop ni nzuri sana  kwaajili ya kuhariri (edit) picha, au kutengeneza mabango ya matangazo ya sanaa kama vile wasanii, muziki n.k. ndio utaona mtu amepiga picha chumbani lakini kwa kutumia Photoshop amewekwa bafuni. Au mtu anapiga picha porini halafu anatumia photoshop kujiweka katikati ya miji mikubwa duniani. Illustrator ni nzuri kwa wanaotengeneza michoro wenyewe upya, unaweza kutumia program hii kuchorea, kutengeneza vitu mbalimbali vyenye kuvutia kama vile mandhari, pia unaweza kutumia hii kutengeneza Business cards, post cards, CD/DVD covers na mengi katika hayo. Lakini kumbuka kuwa kila mtaalamu anaweza akatumia program anayoona kwake ni rahisi, na zote hizo zinaingiliana ni wewe tu na ujuzi wako.

 

Na program za kufanya graphics zenye kujongea (motion graphics) ni kama vile Adobe Flash, Adobe After Effect. Ila Adobe Flash ni kwa graphics za ndani ya website, ndio maana utaona picha na maandishi yakitembea huku na huko katika tovuti mbalimbali hasahasa zile za sanaa na kubadilika rangi n.k

 

Sasa unaweza kujiuliza hapa, "Mimi nimesomea Graphic Designing na nimefaulu na kupata cheti kizuri tu lakini mbona siwezi kutengeneza kama wenzangu wanavyofanya?” Jibu la hapa ni rahisi sana na ni vema ukasoma kwa makini makala hii ili upate ufumbuzi wa tatizo lako.

 

Kusomea Graphic Designing haina maana kwamba ndio tayari umeshajua kuwatengenezea watu kile wanachotaka. Hapa unafundishwa jinsi ya kutumia hizi program kwa mbinu mbalimbali na kufundishwa jinsi ya kutumia zana zake (tools) kama vile kufuta, kuandika, kuchora mstari, boksi, duara, kujaza rangi, upangiliaji mzuri wa rangi, kukuza unene wa mstari na staili tofauti za maumbo, kupangilia kazi yango vizuri katika utengenezaji, kupimia ukubwa wa document yako kama vile A4, A5, B4 na mengi tu zaidi ya hayo niliyoyataja. Na ndio hayo hayo unayofanyiwa mtihani.

 

 

Akili ya ziada inasaidia hapa katika kutengeneza kitu unachohitaji kwa mfano anaweza kutokea mtu akahitaji umtengenezee tangazo linalohusika na kitu fulani, unachotakiwa hapa ni kufikiria jinsi gani upangilie kazi yako na utumie rangi za aina gani, picha gani na maandishi gani ili muonekano wake uvutie. Sio tangazo linahusika na mauzo ya gari wewe unaweka picha ya mwanamke mrembo, au tangazo ni la mauzo ya urembo (cosmetics) wewe unaweka picha za magari au unaweka picha zisizoendana kabisa na tangazo hilo.

 

Kumbuka kuwa upangiliaji wa rangi ni jambo muhimu sana katika kazi hii kwani, kuna rangi hazileti muonekano mzuri na hufanya picha iwe na noise, kelele (sio kelele za kuongea) hapana, kitaalamu hapa noise inajulikana kama vurugu vurugu na mpangilio mbaya wa graphics unazotengeneza.

 

Unapaswa uwe kila siku unatengeneza kazi yako mwenyewe kwaajili ya kujizoesha, unaweza tu kuamua utengeneza Business Cards, Bill Boards (Mabango ya matangazo) au kuhariri picha yako mwenyewe na kuweka hili na lile, hii itakusaidia kukuza ujanja wa kutengeneza graphics kwa mbinu mbalimbali, pia hii itakusaidia kujua uko katika hatua gani ya ujuzi wako na ni vema kuwaonyesha watu makini kazi yako ili wakupe ushauri juu ya muonekano wake, kwani huwezi kujifunza bila kukosolewa na kupata ushauri.

 

Vile vile ushauri mzuri ni kuangalia kazi za wengine halafu ukaiga kuzitengeneza kama zilivyo ili kujipa mazoezi na kuamsha mbinu mbalimbali za kutengeneza kazi hizi. Unaweza kuangalia matangazo mbalimbali, ukaanza kuyaiga kuyatengeneza upya, kisha ukishaweza hili basi unaanza kubadilisha muonekano fulani hivi ambao unauhitaji. Hii itakuza ujuzi wako.

 

Ni vema kutengeneza kazi ambayo umeibuni akilini na usiige kazi ya mtu kwa kumtengenezea mtu mwengine bali iga kwa kufanyia mazoezi tu. Kuiga kazi ya mtu ni kuvunja haki miliki ya mwenye kazi yake.

 

Hifadhi mazoezi yako yote unayofanya na usiyafute hata kama utakosolewa au mwenyewe kuyaona mabaya, hii itasaidia kujilinganisha leo na jana. Vile vile wengi hupenda kuona kazi zako za nyuma ili waweze kukuajiri au kukupa kazi hivyo jiandae sana kwa hili kwa kufanya kazi nzuri kisha ukazihifadhi kwa faida yako mwenyewe.

 

Ikiwa unahitaji ushauri na hujui nani atakupa ushauri juu ya kazi yako basi hakuna tatizo sasa, unaweza kutuma kazi yako kwetu kwa email: staryte.inc@gmail.com ili tuiangalie na kukushauri ili kuboresha ujuzi wako zaidi na zaidi na kukupa mbinu mbalimbali. Na tutaifuta kazi yako baada ya kuona na kukushauri ili kulinda haki miliki yako.

 

Kwa maoni, maswali na ushauri jisikie huru kutuandikia katika kisanduku hapo chini.

Category: COMPUTER | Added by: Admin (22/May/2013)
Views: 3391 | Comments: 2 | Tags: Photoshop, photo, tengeneza, kazi, graphic, designer, tangazo, kadi, shop, Computer | Rating: 2.3/3
Total comments: 2
1 alimaslim  
0 Spam
habari kiukweli ashkuru kwa kuona kitu kama hiki kwa lugha yetu ya kiswahili. lkn pia ningependa kua kuandaa masomo kupitia hii blog yenu itapendeza zaid .

2 Admin  
0
Nzuri sana.. tunashukuru sana kwa maoni yako. Ukitaka kuandaa unaruhusiwa kufanya hivyo. Cha msingi ni kujisajili na utachagua group ya teachers kwenye usajili ili uweze kuwa unapost masomo yako. KARIBU SANA

Name *:
Email *:
Code *: