Home » Articles » EDUCATION

MBINU MPYA ZA UTAPELI NDANI YA MTANDAO

MBINU MPYA ZA UTAPELI NDANI YA MTANDAO

 

Baada ya mbinu za kizamani za kutapeli ndani ya mtandao wa internet, sasa kuna mbinu zilizoboreshwa zaidi kuhakikisha unakosa imani ya kuwa unaweza kutapeliwa. Imekuwa ni rahisi sana kuamini kuwa email address yako inaweza kujulikana popote pale na hivyo kuona kuwa ni rahisi hata mtu kukufikia kimawasiliano hata awe sehemu gani duniani.

 

Kama tulivyoelezea mbinu za utapeli hapo awali katika makala zetu zilizopita, hivi sasa mbinu hizi zimeboreshwa zaidi kuhakikisha mtu anapunguza imani za kutapeliwa. Hii inatokana na sisi kujisahau sana, na kama tukiwa makini basi mbinu hii mpya haiwezi kufanikiwa kwako.

 

Kutokana na kwamba mawasiliano kwa njia ya mtandao wa internet  ni ya ulimwengu mzima, na pamoja na hayo pia ukuaji wa mitandao ya kijamii, hivyo mtu huwezi kuona ajabu au jambo geni pale unapopokea email kutoka katika nchi ya mbali sana.

 

Lakini sasa siku hizi unaweza kuwa umekaa, mara ukasikia sms inaingia katika simu yako ikiwa na ujumbe kama huu "umejishindia $200,000 katika promotion ya iPhone 4 hivyo tuma dai lako katika email hii (unapewa sasa hiyo email)” maneno hayo nimeyatafsiri lakini huja kwa lugha ya kiingereza.

 

Hapo ni uhakika kuamini kwa sababu unaweza kujiuliza swali hili: "Hii namba ni ya nje, na sina ndugu huko wala rafiki, hivyo nani atakuwa amewapa hawa? Huenda ni kweli hii promotion”.

 

Lakini hebu kumbuka kitu kimoja, wakati unajaza taarifa za profile yako katika mtandao wa kijamii kama vile facebook uliweka nambari yako ya simu katika Contact information? Kama ni hivyo basi usione ajabu kupokea sms kama hizi, kwasababu, mwenye nia ya kutapeli huwa anabahatisha mtu yoyote yule ulimenguni kwa kutafuta jina lolote analopenda katika mtandao wa kijamii, kwamaana ukiandika kwa mfano "Alex” basi zitakuja taarifa za Alex wote ulimwenguni waliojiunga na mtandao huo, hivyo wao huangalia nani ana sifa za kuwa na uwezo fulani hata akaweza kutapeliwa. Ndio hapo sasa watu wanapopatikana.

 

Hivyo nakushauri sana kutokuweka taarifa zako muhimu za mawasiliano katika mtandao wa kijamii kuepuka usumbufu na kupata message zenye kukera kama hizi.

 

Mbinu nyingine ni hii na sasa ndiyo imeibuka hasa, unaweza kutumiwa maombi ya urafiki (Friend Request) katika mtandao wa kijamii na hasa wanaume ndiyo hukumbwa na hili. Na anayekuomba ni mwanamke. Baada ya kukubali (accept), anakutumia message ya kwanza ya kukusalimia na kisha zinazofuata halafu angalia uone namba yako ya simu inavyotekwa kirahisi. Angalia mfano hapa chini:

 

(tuchukue mfano huyo anaitwa "someone”)

 

Someone: hi, thanks, how r u doin?

Someone: anyway what r u doing 4 work?

Someone: oooohh!! I have to go offline nw, sorry may be give me ur phone number I’ll Text u later. Byeee!!

 

Sasa hapo ndiyo namba yako ya simu inapotoka kirahisi sana, na sio kwamba ukishaitoa utatumiwa hiyo text anayosema, hapana, unaweza kusahaulishwa hata mwezi mzima au hata miezi, kisha baadaye wakati umejisahau ndiyo unaanza kupokea sms za kujishindia zawadi kabambe kabisa, tena sms ya kutoka nchi ya mbali huko, hapo lazima uamini tu.

 

Baada ya kupokea sms na kukwambia uende katika email yao waliyokupa, ndiyo hapo sasa unapoanza kupelekwa taratibu katika hatua za kibenki na baadaye ndiyo unaambiwa ili upate fedha zako, tuma kiasi cha $350 katika akaunti yao wanayokupa. Ukilinganisha kiasi unachotakiwa kutuma na kile utakachopokea basi huoni ugumu kuzituma kwani zitarudi mara elfu moja na hata kama huna utakopa kwa mtu tu, na tena kwa ile imani ya kupokea mamilioni ya fedha unaweza hata kumuahidi huyo unayemkopa kuwa utamrejeshea mara mbili ya fedha hiyo atakayokukopa.

 

Lakini hakuna sheria yoyote duniani hapa ya kwamba hupokei fedha mpaka utume fedha huo ni utapeli hivyo kuweni makini sana.

 

Kwa maswali, ushauri au maoni, jisikie huru kutuandikia katika kisanduku hapo chini.


Category: EDUCATION | Added by: Admin (23/May/2013)
Views: 1186 | Comments: 1 | Tags: mbinu, mpya, mtandao, ndani, Utapeli | Rating: 0.0/0
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: