Home » Articles » HEALTH

FAHAMU UMUHIMU WA SAIKOLOJIA YA ELIMU

FAHAMU UMUHIMU WA SAIKOLOJIA YA ELIMU


Unaweza kuwa umeshawahi kusikia neno SAIKOLOJIA mara nyingi sana, Lakini hebu tufafanue zaidi kwa yule ambaye hafahamu maana yake. Kwa kifupi kwanza hili neno ambalo asili yake ni kigiriki likiwa na maana ya kwamba, saiko ni mambo yanayohusu akili au ubongo, na lojia ni mambo yanayohusu elimu. Hivyo kwa ujumla tunaweza kusema kwamba saikolojia ni elimu inayohusu mambo ya akili au ubongo.

Somo hili la saikolojia linahusu jinsi wanyama na binadamu wanavyoweza kutumia akili au ubongo katika kumiliki na kuongoza vitendo na tabia zao.

Ni wazi kuwa wanyama wote wana ubongo Lakini ni binadamu peke yake ndiye mwenye uwezo wa kujifunza kwa kutumia ubongo wake wakati wanyama wengine hujifunza kwa kutumia silika na mazoea. Na hii humfanya binadamu kuwa tofauti na viumbe wengine.

Sehemu kubwa ya saikolojia inahusu jinsi binadamu anavyoweza kutumia ubongo au akili yake katika kujifunza, kufikiri na kudhibiti tabia zake.

Kwa ujumla ni kwamba saikolojia ni taaluma ya kisayansi inayohusu tabia/mienendo na michakato ya ubongo au akili ya binadamu katika kujifunza. Tabia au mienendo ni kila kitu ambacho mtu hufanya na ambacho huweza kuchunguzwa moja kwa moja.

Tumeangalia kwa ufupi sana maana halisi ya saikolojia, sasa je unaelewa nini kuhusu saikolojia ya elimu?

Kuna matawi mbalimbali ya saikolojia kama vile saikolojia ya Elimu, Saikolojia ya Kliniki, saikolojia ya Biashara, saikolojia ya Kijeshi  n.k. hivyo basi katika mada hii tunaangalia maana ya saikolojia ya elimu na umuhimu wake.

Saikolojia ya elimu ni tawi la taaluma ya saikolojia linaloshughulikia masuala ya elimu, tawi hili linachunguza jinsi mwanafunzi anavyojifunza mambo mbalimbali ya kielimu, kijamii na kiutamaduni na namna bora ya kumfundisha. Sasa hebu tuangalie tawi hili lina umuhimu gani? Au kuna umuhimu gani wa mwalimu kujua saikolojia?

Umuhimu wa saikolojia ya Elimu

  1. Hii humsaidia mwalimu kujua tabia za mwanafunzi na kujua ni kwa njia au mbinu gani anaweza kuzitumia ili tendo la kujifunza litokee na pia kujua sababu zinazoweza kufanya tendo la kujifunza lisiimarike mfano wanafunzi hutofautiana sana kutokana na malezi waliyolelewa au mahala walipotokea, hivyo kama mwalimu ukishajua tofauti hizi utajua utumie mbinu zipi ili kuhakikisha kuna usawa wa elimu au ulichokifundisha kimeeleweka kwa wote bila ya kubagua mwenye uwezo mkubwa au mdogo.
  2. Husadia pia kujua jinsi ubongo au akili ya binadamu inavyotumika katika tendo la kujifunza. Kujua huku kutafufua njia na mbinu mbalimbali kuhakikisha kinachofundishwa kimefanikiwa.
  3. Husaidia kumjua vema mwanafunzi wako na kujua jinsi gani utamsaidia  ili ajifunze vema zaidi.
  4. Itakusaidia kufahamu matatizo yanayokwamisha mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji na kujua jinsi gani utaweza kuyatatua.
  5. Kwa kufahamu saikolojia na tabia za wanafunzi wako utaweza kuwaandaa vema na kuwapa motisha ili walipende somo na kuwachochea inapobidi. Mfano unaweza kutumia mifano mizuri ya kile wanafunzi wanachokipenda ili kuwafanya wawe na furaha na umakini na kile unachokifundisha.
  6. Utajua kama mwanafunzi ameelewa au hajakuelewa hata kama amekaa kimya bila ya kukuuliza au kusema lolote. Kuna wanafunzi huwa na uoga wa kuuliza swali pale anaposhindwa kuelewa sehemu fulani, hivyo kama una ujuzi wa saikolojia hali hii unaweza kuigundua kwa wanafunzi wako na kuirekebisha.

Kwa upande wangu nina hayo machache, ikiwa una lolote la kuongezea jisikie huru  kuacha maoni yako kwani tuko pamoja katika kuelimisha jamii katika mambo mbalimbali.

Category: HEALTH | Added by: Admin (29/Sep/2013) | Author: Yahyou M. Yahya E W
Views: 12138 | Rating: 1.9/34
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: