Home » Articles » HEALTH

MAHITAJI NA KAZI YA SUKARI MWILINI

MAHITAJI NA KAZI YA SUKARI MWILINI


Sukari ni moja katika familia ya Carbohydrates.

Carbohydrates ndio chanzo kikuu cha nguvu katika miili yetu. Hata hivyo, sio kwamba carbohydrates zote zinaweza kunyonywa au kutumiwa na miili yetu kama ilivyo. Kabla ya kuendelea hebu tuangalie aina za carbohydrates.

Carbohydrates ina aina kuu tatu, Monosaccharides, Disaccharides na Polysaccharides.

Monosaccharides kwa jina lingine hujulikana kama sukari rahisi (simple sugar) ambayo humeng’enywa moja kwa moja bila ya kuvunjwa vunjwa katika mfumo wa mmeng’enyo.

Aina hii ya sukari hutokea katika matunda, mbogamboga na asali. Kutokana na kwamba aina hii haihitaji kuvunjwavunjwa basi humeng’enywa haraka sana na kuingia katika mfumo wa damu mapema sana pindi tu mtu atakapoila.

Aina ya pili ni Disaccharides ambayo huhitaji kuvunjwa vunjwa ili iwe katika mfumo wa monosaccharides ili iweze kumeng’enywa.

Aina ya tatu ni Polysaccharides, hii huundwa kwa molecule nyingi sana za monosaccharides. Vyakula vya wanga huja katika mfumo huu kama vile ngano, mchele, mahindi, viazi, maharage, mtama n.k.

Ile sukari ambayo bado haijabadilishwa au kuvunjwa kwa jina lingine hujulikana kama Glycogen

Glycogen huhifadhiwa katika ini na misuli na hii hutokea ikiwa glucose imezidi mwilini hivyo hubadilishwa kuwa Glycogen na kuhifadhiwa katika ini na misuli. Na hutumika pale mwili unapohitaji nguvu zaidi au Glucose inapopungua, hivyo ile Glycogen iliyohifadhiwa hubadilishwa kuwa Glucose na kutumika katika mwili.

Katika mfumo wa mmeng’enyo, Polysaccharides na Disaccharides huvunjwa vunjwa na kuwa Monosaccharides au sukari rahisi ambayo hunyonywa na damu. Ini hubadilisha Monosaccharides zote kuwa Glucose ambayo baada ya hapo husafirishwa mpaka katika seli za damu.  Glucose huchomwa na Oxygen katika seli za mwili ili kuleta nguvu na kufanya mwili uweze kufanya kazi yake.

Inabidi pia ijulikane kuwa sio kwamba tu sukari tunayokula ndiyo huongeza sukari mwilini Lakini wanga pia huongeza sukari mwilini ambayo kwa mwanzo wakati unaila huwezi kuhisi utamu hata mara moja, Lakini ikishameng’enywa hubadilishwa katika sukari na kuongeza sukari katika damu.

Ikiwa Glucose itazidi mwilini, basi sehemu ya Glucose hubadilishwa kurudi katika Polysaccharides (Glycogen) na kuhifadhiwa katika ini na misuli. Ikiwa Glucose itapungua sasa, ndipo ile Glycogen iliyohifadhiwa katika ini itakapobadilishwa kuwa Glucose na kuendelea kufanya kazi yake.

Kongosho (Pancreas) ni organ inayotoa homoni ya Insulin, insulin ni homoni ambayo kazi yake kubwa ni kudhibiti kiwango cha sukari mwilini, kama kiwango kikizidi basi hupunguza mpaka idadi yake inayohitajika, na kama ikipungua basi hurekebisha mpaka kufikia idadi yake inayohitajika mwilini.

Kupungukiwa na homoni ya insulin ndiyo hufanya kiwango cha sukari kutodhibitika, kiwango cha sukari katika damu kinapozidi 180mg/100ml, hali hii huitwa hyperglycaemia na ndio mtu hupata kisukari (Diabetes). Katika hali hii kiwango cha glucose huwa kikubwa sana kiasi ambacho figo ambazo huwa zinarudisha kiwango cha sukari katika mwili, hushindwa kudhibiti kiasi kinachozidi sana na ndio maana sukari huonekana katika mkojo.

kiwango cha sukari katika damu kinapokuwa chini kufikia 70mg/100ml, hali hii huitwa hypoglycaemia na ndio baadhi ya viungo vya fahamu hushindwa kufanya kazi na mtu kukosa nguvu na fahamu kupotea.

Sukari ina umuhimu sana katika mwili wa mwanadamu Lakini hii haina maana kwamba ndiyo tule sukari hovyo au tule sukari yoyote ile bila mpangilio maalum. Kinachojali zaidi ni ubora na kiwango unachoingiza katika mwili. Kuna sukari ambayo ina madhara katika mwili na moja wapo ni sukari nyeupe.

Nakutakia usomaji mwema na kujifunza kila zuri unalohitaji kufahamu katika tovuti hii. Ahsante.

 

Category: HEALTH | Added by: Admin (22/Jul/2013) | Author: Yahyou M. Yahya E W
Views: 1572 | Rating: 1.5/2
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: