Home » 2017 » November » 5 » Alibaba na wezi 40 Part 9
17:59
Alibaba na wezi 40 Part 9

SEHEMU YA TISA

Kutoka sehemu ya nane:

Sasa nyumba ya Kassim imeshajulikana na mwizi ambaye alikuja mjini kuitafuta, kutokana na kuwa nyumba zote za mtaa ule zilikuwa zikifanana, mwizi akaona ni njia nzuri aweke alama ya chaki kwenye mlango wa nyumba ya Kassim ili asipotee atakaporudi mara nyingine. Lakini hata hivyo, Marjane anakuja kuona alama hiyo na kuamua kuweka alama hiyohiyo katika kila mlango wa nyumba zote zilizopo katika mtaa ule.

ENDELEA SEHEMU YA TISA

Yule mwizi akarudi msituni akimpiga farasi wake ili azidishe mwendo na awahi kufika. Alipokaribia kufika tu kule msituni walipo wenzake akaanza kupiga kelele za kushangilia, “Nimeshaipata nyumba!, nimeipata nyumba!”

Kiongozi wa wale wezi akageuka kumtizama aliyekuwa akija mbio na farasi. Alipomuona ni yule mwenzao akatabasamu.

“Vizuri sana!” akasema kiongozi wao. “Sasa tunaweza kwenda kumtafuta aliytetuibia dhahabu zetu!”.

Yule mwizi akashuka kwenye farasi wake.

“Ilinichukua muda mrefu sana” alisema yule mwizi. “niliongea na mamia ya watu mjini. Nilikwenda sokoni, mpaka kwenye vibanda vya kuuzia kahawa, nilikwenda sehemu mbalimbali lakini hakuna hata mtu mmoja aliyefahamu kuhusu habari ya mtu aliyekufa. Baadaye nikaenda katika kibanda cha mzee mmoja mshona nguo.

“hapo sasa ndipo bahati yangu ilipotokea” aliendelea kuelezea. “Fundi cherehani – jina lake Mustafa – akaniambia kwamba alishona suti ya marehemu katika nyumba moja hapo mjini. Nikamuomba anipeleke hapo nyumbani, lakini akaniambia kwamba alipelekwa huko hali ya kuwa amefungwa kitambaa machoni ili asipajue. Hivyo na mimi ikabidi nimfunge hivyohivyo na kaniongoza mpaka kwenye hiyo nyumba. Aliweza kunifikisha kwenye hiyo nyumba kwa kusikiliza sauti na harufu mbalimbali. Nimeweka alama ya chaki kwenye mlango wa nje wa nyumba hiyo ili iwe ni rahisi kuijua nyumba hiyo tukirudi tena.”

Wale wezi waliposikia hivyo walijipongeza kwa kugongana mikono na miguu.

“Sasa tunaweza kumkamata yule mwizi mwengine!” kiongozi wao alisema. “Twendeni mjini tukiwa katika makundi mawili au matatu tu ili watu wasije kutushtukia. Kisha akamgeukia yule mwizi aliyeigundua nyumba ya Kassim na kumwambia “nitaenda kwenye hiyo nyumba na wewe. Kisha nitaamua nini cha kufanya. Sote tutakutana mjini.”

Hivyo basi wezi wote wakaondoka katika makundi matatu tofauti. Kiongozi wa wezi na yule mwizi wakafika kwenye mtaa ambao nyumba ile ilikuwepo. Mwizi akaonesha kwa kidole chake na kuongea kwa furaha.

“Hii hapa!” alisema mwizi. “Hii ndio nyumba yenyewe. Umeona alama ya chaki mlangoni?”

Kiongozi wa wezi akaenda mpaka karibu na mlango na kuangalia alama ya chaki. “Ndio, Naiona alama ya chaki.” Alisema. “Lakini hebu angalia -  naona kuna alama nyingine tena ya chaki kwenye mlango wa nyumba nyingine- na ile nyingine pia – na ile pia!!!” akawa anatembea nyumba hadi nyumba na kuona kila nyumba mlango wa nje una alama ile ile. Hali hiyo ilimuudhi sana na kumfanya amkasirikie yule mwizi aliyewaleta huku.

“Wewe ni mpumbavu sana!!” Kiongozi alisema. “hii imekuaje sasa, kwanini kuna alama ya chaki katika milango ya kila nyumba, ni nani ameziweka?”

“Sijui Mkuu!” alijibu yule mwizi akiwa hana furaha. “Mimi niliweka lama kwenye mlango mmoja tu”

“Wewe ni mjinga sana! Umeshindwa kazi yangu.” Alifoka kiongozi.  “Sasa kwa hali hii kila mlango una alama hiyo hiyo, sisi tutajuaje hiyo nyumba yenyewe. Aaaghh! Turudi tu kazi imekushinda”

Asubuhi ya siku iliyofuata, wezi wote walikuwa kwenye kikao kingine tena kule msituni.

“Mmoja wetu alishindwa kufanya kazi yangu.” Kiongozi wao aliwaambia. “Lakini ni lazima tuitafute hiyo nyumba. Nani mwingine anaweza kujaribu?”

Wote walikaa kimya Kwa muda mfupi kidogo. Kisha mwizi mwingine akajitokeza mbele. “Mimi nitakwenda,” Alisema.  “Nina uhakika nitaipata hiyo nyumba. Nitaenda kuongea na yule yule fundi nguo, Mustafa”

Haraka sana yule mwizi mwingine akaelekea mjini mpaka kwa fundi Mustafa. Muda sio mrefu yulemwizi akafanikiwa kukiona kibanda cha Mustafa. Yule mwizi akampa mkono wa salamu Mustafa na kumuonesha sarafu ya dhahabu.

“Najua uliwahi kushona suti ya marehemu fulani katika nyumba moja hapa mjini.” Alisema yule mwizi. “na jana ulimpeleka rafiki yangu katika hiyo nyumba, na kaweka alama ya chaki katika mlango ili asiweze kuipoteza katika kumbukumbu yake. Lakini kwa bahati mbaya kuna mtu aligundua hiyo alama na kuweka alama kama hiyo katika kila mlango wa nyumba, hivyo tumeshindwa kuifahamu. Naomba unipeleke katika hiyo nyumba uliyoshona suti ya marehemu, lakini, mimi nitaweka alama ya chaki nyekundu kwenye fremu ya dirisha, alama hiyo itakuwa ndogo sana kiasi ambacho hakuna yeyote atakayeweza kuiona.

Mustafa akaiangalia ile sarafu ya dhahabu. “Ukinilipa vizuri, nitakupeleka.” Alisema.

“Nitakulipa vizuri.” Mwizi alimjibu. “lakini utavaa kitambaa machoni kama ulivyofanya mwanzo.”

Mwizi akachukua kitambaa chekundu na kumfunga nacho Mustafa machoni na kisha wakaanza safari.

Baada ya muda mfupi, Mustafa akasimama na kuvuta harufu. “samaki!” Mustafa alisema. “napenda sana harufu ya samaki akipikwa! Mke wangu huwa ananipikia samaki kila Jumamosi. Hapa lazima tukate kushoto.”

Dakika chache baadaye, akasema Mustafa. “Huyo mbwa anabweka! Nafikiri ana njaa na anataka chakula chake cha jioni. Tuifuate hiyo sauti kisha tutakata kulia.”

Kisha tena baadaye kidogo akasema, “Naukumbuka huu muziki, kuna mtu huwa anapenda sana kuchezea zumari na filimbi  maeneo haya kama nilivyosikia mara ya kwanza. Nafikiri tunakaribia kufika.”

Mwishowe kabisa kwa mshangao, “Waridi! Oooh! Napenda sana harufu ya haya maua, na hapa nina uhakika ndipo kwenye hiyo nyumba, tumeshafika.”

Harufu ya maua hayo yalikuwa yakitoka kupitia kwenye dirisha moja la nyumba ya Kassim. Hiyo ndiyo nyumba ambayo Alibaba, mkewe, mtoto wake, mke wa Kassim pamoja na mfanyakazi wao Marjane walikuwa wakiishi.

“Ahsante sana!” alisema Yule mwizi. “umenifanyia kazi nzuri sana mzee wangu.” Kisha akampa sarafu zaidi za dhahabu.

Mwizi alitabasamu huku akienda kwenye dirisha la nyumba hiyo na kuweka alama ndogo sana ya chaki nyekundu kwenye fremu ya dirisha hilo.

“Hakuna mtu atagundua alama hii ndogo sana,” alijisemea mwizi. “Kiongozi atanifurahia sana!” Kisha akamrudisha Mustafa kwenye kibanda chake cha kushonea nguo naye akarudi kuelekea msituni.

Endelea sehemu ya kumi ya hadithi hii…………….

 

Category: Stories & Entertainment | Views: 718 | Added by: badshah | Rating: 0.0/0
Total comments: 8
7 akidas  
0 Spam
Sir weka party 10

8 badshah  
0
party 10 is ready, didnt you see?

6 shaitu  
0 Spam
Ni tamu sana utadhani ivory. smile biggrin smile biggrin

3 mariana  
0 Spam
Mimi tayari Niko bowad sir please put another story.

4 Admin  
0
Mariana hujaifuatilia tangia mwanzo ndio maana. But dont worry kuna short stories nitaweka.

2 barbie  
0 Spam
Nimeipenda nishasoma

1 fetty  
0 Spam
Mmmh, jaman inaishia pazur....wataman iendelee tu....

5 hafsa  
0 Spam
Jinsi ilivyonzuri naona fupi natamani iendelee

Name *:
Email *:
Code *: