Home » 2018 » January » 13 » SAFARI 7 ZA AJABU ZA SINDUBAD (Part 2)
11:59
SAFARI 7 ZA AJABU ZA SINDUBAD (Part 2)

SINBAD BAHARIA NA SAFARI ZAKE SABA

SEHEMU YA PILI

SAFARI YA KWANZA

Kutoka sehemu ya kwanza:

 

Baada ya Hindubad kulalamika na umasikini wake, tajiri Sindubad aamua kumuita na kumwambia kuhusu utajiri wake kwamba hakuupata kirahisi kama anavyodhani mtu yeyote. Kwa kumthibitishia hivyo, Sindubad aamua kuanza kumhadithia yaliyomsibu katika safari zake saba. Akaanza kuhadithia safari ya kwanza: endelea............

 

Baada ya wote waliohudhuria katika ukumbi ule kuwa tayari kusikiliza, Sindubad akaanza kuhadithia.......

 

“Baba yangu alikuwa ni mmoja kati ya matajiiri wakubwa sana katika mji huu wa Bagdad, na mimi ndiye nilikuwa mtoto wa pekee, sikuwa na ndugu yeyote. Alipofariki aliniachia urithi mkubwa sana. Na nilikuwa kipindi hicho ni kijana mdogo mwenye nguvu.

 

Basi nikachukua mali ile na kuitumia pamoja na marafiki zangu, tukawa ni wenye kula tunachokitaka, tunafanya starehe nyingi zenye kuharibu mali bila ya kutambua kwamba ubadhilifu huu wa mali ipo siku utaisha.

Ghafla siku moja nikagundua kwamba mali yangu haikubaki isipokuwa kidogo sana. Nikaona kwamba nikibakia na hali kama hii nitapoteza kila kitu ninachokimiliki na itakuwa akiba yangu ni kufilisika na maumivu. Na watu wanaonijua hapa mjini huenda wakanisema sana.

 

Hali ile iliniogopesha sana na nikaona naelekea kabisa kwenye mwisho mbaya, nikajiambia katika nafsi yangu, “hakika ufukara wa kujitakia katika mwisho wa maisha ya mwanadamu – matarajio yake ni aibu kwa watu hali ambayo mwenye akili hawezi kuridhia, na hakika uvivu ni ufunguo wa ufukara.”

 

Hivyo nikaazimia kusafiri kwaajili ya biashara. Nikauza kila kilichobaki katika mali yangu na nikanunua kutokana na pesa hiyo bidhaa. Nikasafiri pamoja na wafanya biashara wengine.

Tulianza safari kutoka katika mji wa Bagdad mpaka tukafika katika mji wa Basra ambapo tulipanda meli kubwa iliyosafiri kupitia katika ghuba ya Fursi.

Na hii ndiyo ilikuwa safari yangu ya kwanza, nilikuwa sijazoea kabisa kusafiri baharini mpaka nikaanza kupata homa na kichefuchefu, lakini hali ile ilipotea baada ya muda mfupi tu.

Meli yetu ilikuwa ikitupitisha kisiwa baada ya kisiwa, mji baada ya mji. Na sisi tulikuwa tukiuza na kununua katika vituo vyote hivyo.

Wakati tukiwa njiani baharini, kwa mbali tukaona kisiwa kidogo kimejitokeza kwa juu ya bahari, tukakikaribia, wakashuka baadhi ya wafanyabiashara kwenye kisiwa hiko na mimi nikashuka nao. Tukakaa katika kisiwa hiki muda mrefu kidogo tukiwa tunacheza na kupiga stori mbalimbali mpaka ikafika jioni. Basi tukachukua baadhi ya kuni ambazo tulikuja nazo kwenye meli yetu, kisha tukakoka moto ili tupike chakula.

Muda mfupi tu wakati tunakoka moto, mara tukasikia kisiwa kinatetemeka mtetemeko mkali sana. Hali ilitupa mfadhaiko na hofu, basi nahodha wa meli akatuita haraka sana na kutuambia, “njooni haraka kwenye meli kabla hamjazama!!!” na wala nahodha hajamaliza kusema maneno hayo na kisiwa chote kilizama ndani ya bahari mara moja.

Basi walipona wote waliokuwa karibu na meli na waliobakia wote walizama baharini. Kumbe kile hakikuwa kisiwa kama tulivyodhani, bali ni samaki mkubwa sana ambaye alikuwa amelala katika uso wa maji, na tulipokoka moto samaki yule alihisi joto kali sana hivyo aliamka na kukimbilia ndani ya maji. Basi walipona waliojaaliwa kupona na walizama waliopangiwa kuzama.

Ama mimi nilikuwa mmoja kati ya wale waliokuwa mbali na ile meli, hivyo sikupata nafasi ya kuifikia ile meli kwa haraka wakati samaki yule akizama baharini. Ningezama baharini kama wale wenzangu endapo nisingepata bahati ya kushikilia kipande kikubwa cha gogo ambacho tulikuja nacho kwaajili ya kufanya kuni.

Basi niliwaita wenzangu waliokuwa kwenye meli kwa sauti yangu ya juu kabisa, lakini hawakuweza kunisikia kutokana na hofu iliyowajaa. Na nikaona meli ikipotea katika upeo wa macho yangu, nikabaki najiokoa kwa kuogelea kwenye gogo lile huku likipelekwa na mawimbi ya bahari.

Ulipoingia usiku, nikawa na uhakika kabisa kwamba sasa ndio mwisho wa maisha yangu. Lakini niliendelea kujipa moyo licha ya kuwa na tabu na hofu. Nilibaki katika hali hii usiku kucha mpaka kupapambazuka.

Basi nikaona kwa mbali katika upeo wa macho yangu kisiwa chenye miti mirefu mirefu yenye matawi yaliyojitokeza baharini, basi hiyo ikawa ni bahati nzuri imenikuta hapo. Basi nilipokaribia hapo nikarukia tawi la mti mmoja uliojitokeza baharini na nikapumzika katika kisiwa hicho baada ya kupata shida na tabu zote zile.

Na niliishiwa na nguvu nyingi sana kutokana na matatizo yaliyonikuta. Nikalala mchana wote ule na usiku wake wote, kisha nikaamka asubuhi ya siku iliyofuata. Nyayo zangu zilikuwa zimevimba hali iliyopelekea nitembee kwa kutegemea kipande cha mti nilichokikata katika mti mmoja wapo hapo kisiwani.

Nilishikwa na njaa kali sana kiasi ambacho nilihisi kabisa inakaribia kuniua, lakini kwa bahati nzuri nilikuta katika kisiwa kile matunda mengi yaliyoiva na pia nikaona chemchem ya maji ya baridi, nilifurahi sana, nikala mpaka nikashiba na nikanywa mpaka nikaridhika kabisa. Nikaendelea kukaa katika kisiwa kile mpaka jua lilipokuwa linazama.

 

Na baada ya siku chache, udhaifu wote uliondoka na afya yangu ikarudi kama mara ya kwanza. Nikawa katika hali ya kuzunguka katika kisiwa kile. Na wakati niko katika mizunguko yangu pale kisiwani, nikaona kwa mbali kama kivuli cha mnyama ambaye sikujua ni mnyama gani.

 

Basi nikamfuata ili nijue ni mnyama gani, na nilipofika tu nikaona kumbe ni farasi akiwa katika malisho yake na hali ya kuwa amefungwa. Na nikasikia sauti za watu wakizungumza ndani ya pango moja lililopo pale kisiwani. Hali ile ikanishtua sana, na wakati niko katika mshituko huo, mara akatokea mtu mmoja nisiyemfahamu. Akaniuliza sababu iliyopelekea mimi kuwa pale katika kile kisiwa. Nikamuelezea kisa chote, basi kisa kile kilimshtua sana, akanichukua mpaka kwenye pango ambalo alitokea, nikawaona jamaa zake wakiwa ndani wakimsubiria. Basi akawahadithia yale yaliyonikuta kama nilivyomuhadithia.

Wakanikaribisha chakula, nikala na nikanywa. Kisha nikawauliza sababu ya kuja kwao hapa kisiwani na kujificha katika pango. Wakaniambia kwamba, wao ni watumishi wa mfalme Maharaja ambaye ndiye mwenye kile kisiwa, na kwamba kila mwaka huwatuma watumishi wake waende na farasi wa kike kwaajili ya malisho katika kisiwa kile, lengo lake ni kwamba farasi wale wakiwa katika malisho yao hutokea farasi dume wa baharini na kuwapanda farasi wale wa kike.

 

Basi yule farasi wa baharini akijaribu tu kutaka kumchukua farasi wa kike ili akimbie naye baharini basi wanatoka kwenye pango na kumfukuza, naye hukimbia na kutoweka baharini. Kisha humchukua farasi wao na kurudi naye mjini. Na baada ya muda farasi yule wa kike huzaa mtoto anayefanana na farasi wa baharini. Lengo ni kuchukua mbegu za farasi yule wa baharini kwani sio farasi wa kawaida.

Wakati wanamaliza tu kunisimulia sababu ya wao kuwa pale ghafla tukasikia sauti ya farasi wa baharini, basi tukachungulia kwenye tundu la pango ili tuone nje, tukamuona farasi yule akijaribu kumlazimisha farasi wao ili akimbia naye kwa nguvu. Basi wakatoka wote nje ya pango na alipowaona tu akakimbia na kutoweka baharini.

Basi siku iliyofuata, waliondoka pamoja nami mpaka kwenye mji wao wa Hindu. Wakanikaribisha na kunitambulisha kwa mfalme wao Maharaja. Akaniuliza juu ya kisa changu kilichonitokea, nikamuhadithia kila kilichonitokea. Basi alishtuka sana juu ya kisa hicho na alikuwa na furaha na mimi furaha iliyo kubwa sana na akanikarimu na kunikaribisha kwake.

Ikawa katika mji ule zinakuja meli mbalimbali za wafanya biashara kutoka sehemu mbalimbali duniani. Nami nikawa najaribu kila siku kuuliza wafanya biashara wanaokuja juu ya habari za mjini kwangu Bagdad lakini sikuweza kupata habari yolote kuhusu Bagdad. Na ikapita hali ile muda mrefu sana mpaka nikakata tamaa ya kuiona nchi yangu na watu wangu.

Katika maajabu niliyoyaona katika visiwa vilivyozunguka mji wa Hindu ni majoka ya baharini pamoja na samaki wa ajabu wenye urefu upatao mita nne, wengine walikuwa na sura kama za bundi na wengine walikuwa na sura kama za watu. Lakini nikaja kugundua kwamba viumbe hawa wa ajabu hawakuwa na madhara kwani nilipowatishia kama nataka kuwapiga na fimbo walikimbia baharini na hawakutoka tena.

Siku moja nilikuwa nimekaa kando kando ufukweni mwa bahari, nikaona kwa mbali meli iliyokuwa inakuja, ilipofika  ikashusha bidhaa zilizokuwepo. Na nikaona baadhi ya bidhaa hizo zimeandikwa “SINDUBAD”, basi nilipojaribu kumuangalia nahodha wa meli ile nikamfahamu kabisa. Nikamuuliza juu ya mwenye zile bidhaa naye akanijibu kwa huzuni sana, “Mwenye bidhaa hizi ni Sindubad.” Aliendelea kusema. “Alipata ajali na kuzama kwenye bahari pamoja na wafanya biashara wenzake na mimi pia nilikuwepo ila nilisalimika, tulisimama katika mgongo wa samaki mkubwa sana aliyelala tukidhani ni kisiwa, na alipoamka samaki yule basi akawazamisha wote isipokuwa waliokuwa karibu na meli ndio walisalimika, mungu awarehemu wote. Basi nikaamua kuchukua bidhaa zake na kumuuzia kisha kila faida niliyopata nilikuwa nawapelekea jamaa zake kipindi nilichorudi mjini Bagdad.”

Alipomaliza kunielezea, nikamsogelea kwa karibu zaidi na kumwambia, “mimi ndiye Sindubad unayemzungumzia, na hizi ni bidhaa zangu.”

Nilipomwambia hivyo alikunja uso na kwa hasira akaniambia, “Huoni aibu kutaka kuchukua amana za watu? Vipi unajiita Sindubad na hali ya kuwa nimemuona kwa macho yangu akizama baharini?”

Nikamjibu, “usinikasirikie ndugu yangu, na wala ninayoyasema si ya uongo.”

Basi nikamuhadithia kila kitu kuhusu safari yetu tangu tunaanza safari kutoka mjini Bagdad mpaka tukafika Basra, na nikamwambia mambo yote yaliyofanyika katika safari yetu na mazungumzo yetu tuliyokuwa tukizungumza pia nilimwambia na nikampa kisa chote mpaka tukafika kwenye mgongo wa samaki na kuzama.

Kwa maelezo yangu yale aliamini kabisa kuwa kweli mimi ndiye Sindubad, na alifurahi sana kwa kuokoka kwangu katika janga lile na akanikumbatia kwa furaha kubwa sana na wakaja wale waliokoka pamoja na yeye katika meli nao wakanitambua na tukafurahi sana pamoja.

Nilimshukuru sana nahodha yule kwani alifanya uaminifu mkubwa sana kuniuzia bidhaa zangu kipindi chote hicho, na nilimpa kiasi fulani cha thamani ya bidhaa zangu kama shukrani yangu kwake lakini hakutaka kuchukua hata kidogo.

Basi nikachagua zawadi yenye thamani kubwa kisha nikampelekea mfalme Maharaja, akaniuliza. “Umeipata wapi hii?” Nikamuelezea yaliyotokea naye akaniamini niliyomwambia na kwa furaha kabisa kapokea zawadi ile. Kisha na yeye akaamuru nipewe zawadi yenye thamani kubwa zaidi ya ile niliyompa mimi.

Nilipomuomba idhini ya kuondoka na rafiki zangu kurudi mjini kwetu,  akaniruhusu. Na baada ya wenzangu kuwa tayari kwaajili ya safari nikaondoka kwake nikimshukuru sana mfalme Maharaja kwa kukaa na mimi kwa ukarimu sana.

Na nikauza mjini pale kila nilichonacho katika zile bidhaa zangu na kupata fedha nyingi sana na nikanunua badala yake bidhaa nyingine. Na nikarudi mjini kwangu na mali nyingi sana.

Tuliondoka na meli kwa amani kabisa, na bahari ilikuwa imetulia na upepo ulikuwa unapepea kwa upole kabisa na hatukupata tatizo lolote lile mpaka tulipofika mji wa Basra.

Kisha tukatoka Basra mpka mjini kwetu Bagdad pale jamaa zangu waliponiona na kufurahi sana kwa kurudi kwangu salama. Na nikanunua jumba kubwa na vitu mbalimbali vya ndani, nikawa ni mmoja kati ya matajiri wakubwa sana Bagdad. Na nikawasaidia mafakiri na masikini na nikaazimia kutulia katika mji wangu na kuepuka tena safari za baharini na mashaka yake.

Alipomaliza Sindubad kuelezea, akamgeukia Hindubad na kumwambia huku akitabasamu, “Hayo ndiyo yaliyonikuta katika safari yangu ya kwanza, na nitakusimulia kesho yaliyonikuta katika safari yangu ya pili na niliyoyaona katika maajabu ambayo ni zaidi ya safari yangu ya kwanza.”

Hindubad alishtuka sana kusikia hivyo na waliokuwepo pia, kisha Sindubad akaamrisha Hindubad apewe dinari mia moja na kampatia mavazi kadhaa mazuri, kisha akamuombea dua na akaondoka hali ya kuwa ni mwenye kushukuru na mwenye furaha. Na waliokuwepo pia walitoka ili waje kesho kwaajili ya kurudi kesho kwa Sindubad.

Je kuna nini kwenye safari ya pili? Usikose kuisoma sehemu inayofuata.

Category: Stories & Entertainment | Views: 451 | Added by: badshah | Tags: sindubad, safari saba, hadithi | Rating: 3.5/2
Total comments: 1
1  
Part 3

Name *:
Email *:
All smileys
Code *: