Home » 2017 » December » 11 » Alibaba na wezi 40 Part 12
20:00
Alibaba na wezi 40 Part 12

SEHEMU YA KUMI NA MBILI

MARJANE NA MAFUTA

Kutoka sehemu ya kumi na moja:

Kiongozi wa wezi afanikiwa kuingia katika nyumba ya Alibaba na kutokana na mbinu zake Alibaba alimkaribisha kwa ukarimu kabisa na kupata chakula ch ausiku pamoja kwa furaha sana. Sasa alibaba na familia yote inaingia ndani kulala ila kiongozi wa wezi anaamua kuomba ruhusa ya kutoka uwani ili kupata hewa safi ya nje kidogo kabla ya kwenda kulala................

Endelea sehemu ya Kumi na mbili.

Kiongozi wa wezi akatoka nje mpaka uwani. Akasimama mlangoni kwa muda kidogo na akavuta pumzi, kisha kwa taratibu akaanza kuangalia huku na huku ili kuhakikisha kwamba hakuna mtu yeyote anayemtizama. Mbele yake ilikuwa ni ile safu ya mitungi yake aliyokuja nayo ambayo mifuniko yake ilikuwa iko wazi kidogo na ndani yake kuna wezi na walikuwa wamekaa kimya sana.

Akasogea karibu na mtungi wa kwanza, akainama kidogo kisha akaugonga pembeni kwa ishara ya kumuita aliye ndani yake, kisha akafungua mfuniko na kumnong’oneza mwizi wa kwanza kwenye ule mtungi.

“Sikiliza kwa makini!” alimwambia. “Hii ni sehemu inayofuata ya mpango wangu. Ukifika muda wa mashambulizi, nitarusha vijiwe kutoka katika dirisha la chumba nitakacholala. Vitaangukia huku uwani, mkivisikia tu tokeni na panga zenu na mkiwa tayari kushambulia. Nitakuja na mimi kuungana na nyinyi na kisha mwishowe tutamuua huyu Alibaba mwizi wa mali zetu!!”

Yule kiongozi wao alienda kwenye kila mtungi na kuugonga pembeni ili kumuita aliye ndani yake na kumwambia maneno yale yale kama aliyomwambia mwizi aliye kwenye mtungi wa kwanza. Kisha katabasamu na kupangusa mikono yake. Mpango ulikua unaenda vizuri sana.

Akaokota baadhi ya vijiwe na kuviweka mfukoni mwake kisha akarudi ndani ya nyumba na kumuita Marjane.

“Nakwenda kulala sasa,” alimwambia. “Nimechoka sana.”

“Nitakuonesha chumba cha kulala kilipo.” Marjane alijibu.

Marjane akaweka vyombo vyake alivyokuwa akimalizia kuosha na kufuta mikono yake. Kisha akawasha mshumaa na kumuongoza kiongozi wa wezi juu ghorofani kwenye chumba chake. Akafungua mlango  na kumkaribisha ndani.

“Natumai utakaa kwa faraja humu.” Alisema Marjane. “Je, kuna chochote kingine utakachohitaji?

 

“Hapana, Marjane. Nina furaha sana kulala katika kitanda hiki kizuri hivyo nadhani sihitaji kitu kingine. Nashukuru sana!.”

“usiku mwema,” alijibu Marjane. Kisha akarudi jikoni. Akaamua amenye vitunguu na karoti aviweke kwenye sufuria kwaajili ya mlo wa kesho kabisa. Lakini alipochukua kisu tu aanze kumenya mara giza likatanda jikoni.....

“Oooh, chemli imeisha mafuta,” Marjane alijisemea.  Hivyo akachukua mshumaa na kwenda kwenye kabati. Kulikuwa na unga mwingi wa kutosha, mchele na sukari. Lakini kopo la mafuta lilikuwa tupu.

Marjane akavuta pumzi ya kuonesha kuchoka na hali ile ya kukosa mafuta ya kuwashia taa. “Nifanye nini sasa?” alifikiria. “ni usiku sasa maduka yote yamefungwa.

Kisha kapata wazo.

“Kuna mitungi arobaini ya mafuta nje!” alijisemea. “nina uhakika mgeni wetu hawezi kuchukia endapo nitachukua japo kidogo tu kwaajili yakuwashia taa pale nitakapomwambia kesho.” Kisha akachukua kopo la mafuta na mshumaa kisha akaelekea uwani kwenye ile mitungi arobaini. Alipofika akaenda kwenye mtungi wa kwanza uliokuwa karibu naye na kuanza kufungua taratibu mfuniko. Mara akasikia sauti itokayo ndani ya mtungi.

“Vipi muda tayari tutoke kwaajili ya mapambano?” sauti iliuliza kutoka kwenye mtungi.

Marjane alishtushwa na hali ile yenye kushangaza. Akasimama imara na kukaa kimya kwa umakini kabisa.

“Nifanye nini sasa?” alifikiria. “Kuna mtu kwenye huu  mtungi wa mafuta!! Nadhani amekuja na huyu mgeni wetu muuza mafuta. Na sasa yuko tayari kwaajili ya mapambano, nafikiria bosi wangu Alibaba yuko hatarini, lazima nimuokoe.”

“Bado – ila muda mfupi tu nitawajulisha!” marjane alimjibu yule mwizi aliye ndani ya mtungi. Alitumia sauti ya kukaza ili ifanane na ya kiume kama ile ya muuza mafuta. Kisha akaenda kwenye mtungi unaofuata na mambo yakawa ni yaleyale kama ya kwenye mtungi wa kwanza. Kisha akaenda mtungi baada ya mtungi na maswali ya wezi yalikuwa ni yaleyale na majibu ya Marjane yakawa ni yaleyale. “Bado – ila muda mfupi tu nitawajulisha!”

Alipokwenda kwenye mtungi wa arobaini, kulikuwa kimya, hakuna sauti iliyouliza, “Vipi muda tayari tutoke kwaajili ya mapambano?” Marjane akafungua mfuniko na kuangalia ndani ya mtungi akakuta kuna mafuta na kuamua kuchota kwaajili ya taa yake.

Alipokuwa akijaza kopo lake mafuta yale alikuwa akifikiria, “kuna watu thelathini na tisa katika mitungi hii, wako tayari kumshambulia bosi wangu! Yule mgeni ndani atakuwa ni kiongozi wao!”

Kisha Marjane akaamua kuwa na mpango wa kumuokoa bosi wake, Alibaba.

Aliporudi jikoni, aliwasha taa yake na kuchukua sufuria kubwa kabisa na kuliweka jikoni, kisha akamimina mafuta yaliyobaki kwenye kopo. Akarudi kwenye mtungiwa arobaini kwa mara ya pili na kujazalile kopo mafuta na kwenda kuyamimina katika lile sufuria kubwa lililopo jikoni likiwa linaanza kupata moto. Alifanya hivi mara kadhaa mpaka sufuria likajaa mafuta.

Mafuta yalipoanza kuchemka akalitoa kwenye jiko na kulipeleka uwani ilipo ile mitungi. Akafunua mtungi wa kwanza na kumimina yale mafuta ya moto kiasi cha kutosha, kisha kafanya hivyo hivyo katika kila mtungi.

Marjane akarudi jikoni na kumalizia kazi zake za kuandaa mboga ya kesho. Kisha akazima moto na taa.

“Leo siendi kulala,” alijisemea. “ Nitakaa hapa nione nini kitatokea.” Akakaa kwenye stuli karibu na dirisha akitazama uwani kwenye ile mitungi.

Kiongozi wa wezi alijilaza kitandani kwa muda na kusubiri. Alisubiri kwa muda mrefu sana. Baadaye akajisemea, “kwa muda huu kila mtu ndani ya nyumba atakuwa ameshalala.” Kisha akatoka kitandani na kuelekea dirishani,  kisha kwa ukimya kabisa akafungua dirisha. Akaangalia uwani ilipo mitungi na kusikiliza. “Sioni taa yoyote,” alijisemea. “Na sisikii sauti yoyote, sasa nina uhakika kila mtu amelala humu ndani, na sasa ni hatua inayofuata ya mpango wangu. Nitarusha vijiwe kwenye ile mitungi, watu wangu wakisikia tu watatoka na kuanza mashambulizi kama tulivyopanga na kumkamata Alibaba!!”

Akachukua vijiwe alivyokusanya kabla ya kuja kulala na kuvijaza kiganjani na kuvirusha chini kwenye mitungi na akasikia sauti ya vijiwe vikiangukia kwenye ile mitungi. Alisubiri lakini hakuna chochote kilochotokea! Hakuna hata mwizi mmoja aliyetoka kwenye mtungi.

Kiongozi wa wezi akarusha tena vijiwe kiasi cha kujaza kiganja, vikaanguka tena chini na sauti akaisikia lakini kwa mara nyingine tena hakuna kilichotokea na wala hakuna jibu lolote.

Kiongozi wa wezi akaanza kuingiwa na woga sasa. Alihisi tu kuna kitu kimetokea.

Akawasha mshumaa na kushuka taratibu kulekea uwani kwenye ile mitungi yake, akafika kwenye mtungi wa kwanza kisha akafunua mfuniko kidogo.

“Uko tayari?” akauliza. “uko tayari kwa mapambano?” Hakuna jibu. Akajaribu kuvuta harufu. “nahisi harufu ya mafuta humu,” alijisemea. “mafuta ya moto!!”

Akafunua mfuniko wote na kuangalia ndani ya mtungi. Mwizi aliyekuwepo mle ndani ya mtungi alikuwa ameshakufa!!

Kiongozi yule wa wezi akaangalia katika kila mtungi kwa hasira na kukuta wezi wote wamekufa!

“Sijui nini kimetokea,” alifikiri. “Yaani watu wangu wote wamekufa, ina maana kuna mtu amegundua mpango wangu kwa kumshambulia Alibaba. Akaamua kuwaua! Sasa atakuwa nani kafanya hivi?? Alibaba mwenyewe?? Mke wake?? Oooh siko salama tena kwenye nyumba hii yaani nimebaki peke yangu, lazima nikimbie kuokoa maisha yangu.

Kiongozi wa wezi akaacha mitungi yote na punda wote na kuruka kwenye ukuta wa uwani, akakimbia mbio zote kwa kadiri awezavyo. Lakini hakumsahau Alibaba. Alikuwa na hasira sana na bado alihitaji kumuua.

Asubuhi iliyofuata, Alibaba aliamka mapema sana, akachukua  taulo yake na sabuni. Kisha akashuka chini na kukuta mitungi ile bado ipo.

“Ajabu! Hii mitungi bado ipo hapa sasa hivi” alijisemea. “Lakini bado mapema sana labda muuza mafuta bado amelala.”

Kisha Alibaba akaondoka kuelekea bafuni. Hakujua lolote lililotokea usiku ule.

Endelea sehemu ya kumi na tatu ya hadithi hii…………….

 

Category: Stories & Entertainment | Views: 583 | Added by: badshah | Rating: 1.0/2
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: