Home » Articles » HEALTH

HARUFU MBAYA YA MDOMO SABABU NA UTATUZI WAKE.

HARUFU MBAYA YA MDOMO SABABU NA UTATUZI WAKE.

 

Unaweza kujiuliza mbona ukiongea na mtu anakupa nafasi fulani mbali kidogo? Hawezi kuongea na wewe uso kwa uso? Ila ukinyamaza naye husogea kidogo na muonekano wake wa uso unatofautiana pale unapoongea na unaponyamaza? Ukiongea uso wake hubadilika. Kwakweli mdomo ni kitu muhimu sana katika mazungumzo na kinatakiwa kichungwe kwa hali ya juu ili kujenga uhusiano mzuri baina ya mzungumzaji na msikilizaji.

Harufu mbaya ya mdomo humfanya msikilizaji ambaye unaongea naye ana kwa ana kupoteza umakini wote wa jambo unalomwambia na kuanza kufikiria juu ya harufu mbaya ya mdomo. Sasa je? Ni nini hasa kinasababisha mtu kuwa na harufu mbaya ya mdomo? Hebu tuangalie baadhi ya sababu:-

1.    Mdomo mchafu

"Asilimia 90 ya harufu ya mdomoni hutokea kwenye mdomo wenyewe – aidha kutokana na vyakula unavyokula au wadudu ambao wako humo,” alisema dokta Richard H. Price msemaji wa Shirika linaloshughulika na meno. "Harufu ya mdomo ni kama harufu nyingine za mwilini – ni yale matokeo ya viini vya magonjwa kuacha athari sehemu fulani katika mwili.” Mdomoni, hii inamaana kwamba bakteria ambao huishi katika mdomo wa mtu huingiliana na mchanganyiko wa vyakula pamoja na damu na tishu za mdomoni hivyo kusababisha harufu mbaya. Kama huusafishi vizuri, bakteria watajiweka humo na kusababisha harufu mbaya.

2. Ukavu wa mdomo na fizi kuoza

Hali fulani ya mdomo inaweza kuzidisha ukuaji wa bakteria na harufu mbaya, kama vile maradhi ya fizi na ukavu wa mdomo. Maradhi ya fizi husababisha damu kutoka kwenye fizi na matokeo yake kutengeneza bakteria wenye kuozesha. Lakini ukavu wa mdomo ndiyo sababu kubwa kabisa ya harufu mbaya mdomoni kwani mate husaidia sana kusafisha mdomo na kuwasafirisha bakteria kutoka sehemu moja hadi nyingine hivyo hawawezi kukaa sehemu moja na kuzaliana na kuharibu sehemu hiyo.

3. Vyakula vyenye harufu mbaya

Kuna baadhi ya vyakula huwa na harufu nzuri sana pale vinapokuwa nje lakini vinapoliwa na kukaa tumboni baada ya masaa kadhaa hivi kutokana na mfumo wa mmeng’enyo huingia katika mishipa ya damu na kutolewa na pumzi pale unapopumua. Alisema maneno haya Jeannie Moloo, msemaji mkuu wa shirika la mambo ya lishe la marekani (American Dietetic Association). Mfano wa baadhi ya vyakula hivi ni kama vile Vitunguu, vitunguu saumu, Alkohol na tumbaku.

4. Upungufu wa carbohydrates mwilini

Kuzidi kwa Protini na kupungua kwa carbohydrates mwilini husababisha mwili kuunguza mafuta yaliyohifadhiwa mwilini badala ya Carbohydrates na hivyo kusababisha hali inayoitwa Ketosis. Mafuta yanapounguzwa hutokea harufu fulani ambayo hupitia kwa njia ya pumzi na hivyo kusababisha harufu mbaya.

5. Ugonjwa

Wakati mwingine harufu mbaya huweza kuwa ni ishara ya baadhi ya maradhi makubwa. Hasa hasa kisukari au GERD (gastro esophageal reflux disease). Gerd ni ile hali ya acid kuvuja kutokea tumboni mpaka kwenye umio. Na hii huwa ni sababu ya maradhi ya ini au figo – pale sumu inapotoka katika ogani hizi na kwenda moja kwa moja kwenye mapafu na matokeo yake kusababisha harufu mbaya.

 

Je tufanye nini ili kuondoa tatizo hili?

 

1. Safisha mara kwa mara mdomo

Njia ya kuepukana na harufu mbaya ya mdomo kwa asilimi akubwa ni kupiga mswaki, kuchokonoa meno kwa uzi kuondoa vyakula vilivyoganda na kusugua ulimi mara mbili kwa siku, na hasa harufu iliyo safi kabisa siri kuu ni ulimi ulio safi. Hivyo kupiga mswaki, kuchokonoa meno kwa uzi na kusugua ulimi mara mbili ni njia nzuri sana ya kudhibiti harufu mbaya mdomoni.

2. Fanya mdomo wako uwe na unyevu saa zote

Unyevu wa mdomo husababishwa na mate, na njia bora kabisa ya kufanya mate yawe mdomoni ya kutosha ni kunywa maji mengi sana. Hivyo ni vema kunywa maji mengi sana ili kusaidia mate yawe ya kutosha katika mdomo na hii itaepusha ukavu wa mdomo ambao bakteria huzaliana sana.

3. Kuwa makini na  vyakula unavyokula

Epuka kula sana vyakula ambavyo vinaweza kusababisha harufu mbaya kama tulivyozungumzia hapo awali kama vile vitunguu, vitunguu saumu, tumbaku, kahawa na vinginevyo, sio kwamba usile kabisa vitunguu au vitunguu saumu hapana, hivi pia vina faida sana katika mwili na ni tiba ya maradhi mbalimbali Lakini isiwe kila mara au kuzidisha sana.

4. Kula sana matunda

Matunda husaidia sana, itasaidia kuondoa au kuzuia sumu inayotengenezwa katika mwili ambayo husababishwa na kuunguzwa kwa mafuta yaliyohifadhiwa katika mwili ambayo pia ni sababu ya kuwa na harufu mbaya mdomoni.

5. Muone Daktari

Inawezekana ukawa umetumia njia zote hizi za kuzuia harufu mbaya mdomoni lakini harufu ikawa bado ipo, hivyo ni vema ukimuona daktari kwani huenda ikawa ni dalili ya maradhi makubwa kama tulivoelezea hapo mwanzo.

Kwa upande wangu ni hayo tu na huenda kukawa na njia mbalimbali za kuzuia harufu mbaya mdomoni ambazo wengine hutumia siku hizi kama vile kula Big G zenye harufu nzuri ya Mint na kadhalika, lakini si vema kutibu moja na kusababisha jingine kwani unaweza kuondoa harufu ya mdomoni na kusababisha kuoza kwa meno. Ikiwa una nyongeza au maswali au ushauri jisikie huru kutuandikia hapa, tuko pamoja katika kutoa elimu mbalimbali kwa manufaa ya jamii. Ahsante.

 

Category: HEALTH | Added by: Admin (12/Oct/2013) | Author: Yahyou M. Yahya E W
Views: 2129 | Rating: 2.0/1
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: