Home » Articles » HEALTH

YAJUE MANUFAA YA KABICHI KIAFYA

YAJUE MANUFAA YA KABICHI KIAFYA


 

Kabichi ni zao linalolimwa mahala pengi sana hapa duniani. Mboga hii imekuwa ikiwekwa katika hadhi ya chini katika mboga, na hata watu huitumia pale tu wanapoona hakuna jinsi ya kupata mboga ya aina nyingine. Na hivyo utaona ikitumika katika sehemu za jumuiya kama vile shule, magerezani na vyuoni kwani gharama yake ni ndogo hivyo huweza kuhimili hali ya kuinunua kwa matumizi ya watu wengi.

 

Mboga hii ina manufaa mengi sana mwilini lakini iwe ni mpya ya kijani/nyekundu au hata zambarau na siyo ile iliyokaa sana sokoni hadi kusinyaa, hiyo haina manufaa. Mboga hii ina faida zifuatazo:

 

kuondoa sumu mwilini

 

kabichi ina Vitamin C kwa wingi kuliko hata machungwa, pi aina kampaundi za salfa, vitu hivi huisaidia sana kusafisha damu na kuondoa sumu na kupigana na visababishi vya saratani mwilini. Pia huimarisha ini hivyo hulifanya lifanye kazi vizuri.

 

Huzuia saratani

Ulaji wa kabichi huzuia saratani ya matiti, utumbo mpana na saratani ya korodani (testes) kwa wanaume. Kwani ina kampaundi zinazosaidia kupigana na visababishi vya saratani.

 

Huzuia uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo

Mboga hii huondoa lehemu katika damu kwani huleta shinikizo kubwa la  damu pale yanapojaa, na pia huweza kusababisha kiharusi na moyo kupasuka. Hivyo kabichi husaidia kuondoa.

 

Ina Vitamin Muhimu kwa wingi

Kabichi ina Vitamin A, B, C, E na K kwa wingi ambazo zina faida kubwa sana mwilini kama ifuatavyo:

  1. Vitamin A huisaidia kuimarisha ngozi na uwezo wa kuona.
  2. Vitamin B huimarisha uwezo wa kutafakari na kuboresha utendaji kazi wa ubongo na kuzuia msongo wa mawazo.
  3. Vitamin C huimarisha kinga ya mwili na kuzuia visababishi vya saratani.
  4. Vitamin E hufanya ngozi yako kuwa nyororo na kuonekana kijana.
  5. Vitamin K huimarisha mifupa na huhusika na ugandaji wa damu pale unapoumia

 

Manufaa mengine ni kama vile kulinda mwili na maambukizi ya magonjwa mbalimbali,pia hutibu vidonda vya tumbo, kwani utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha tiba cha Stanford ambapo wagonjwa 13 walipona vidonda vya tumbo kwa kunywa juisi ya kabichi mara 5 kwa siku kwa muda wa siku 7 hadi 10. Kabichi pia hutibu michubuko mbalimbali ya mwili.

 

Vilevile huisaidia sana kupunguza uzito au unene kwani ina kiwango kidogo sana cha kabohidreti na mtu anayetaka kupunguza unene na uzito anashauriwa kula saladi ya kabichi kwa wingi.

 

Pia kabichi hupunguza tatizo la kufunga choo kwani ina kambakamba zinazosaidia kulainisha choo na Vilevile ina madini ya salfa na chuma yanayosaidia kusafisha utumbo.

 

Jinsi ya kuandaa kabichi:

Kabichi inapendekezwa sana kuliwa ikiwa mbichi  kwa kuongezwa ndimu na chumvi ili kuleta ladha nzuri kama vile kachumbari, Vilevile unaweza tu ukaichemsha supu yake lakini isiive sana kiasi cha kuua virutubisho vyake, inapendekezwa kuchemka kwa dakika 4 hadi 5 tu. Pia inaweza ikakatwakatwa na kutengenezwa juisi yake kiasi cha kikombe kimoja cha chai kinatosha. Pia inaweza kuchanganywa na mboga nyingine kama vile mchicha au majani ya maboga.

 

Utunzaji:

Kumbuka kuitunza kabichi pale unapotoka kuinunua kwa kuihifadhi katika jokofu (friji) ili isiingie vijidudu. Vilevile kumbuka kuwa kabichi huwa ina tabia ya kuhifadhi vijidudu pale inapotoka shambani au pia huwa na uchafu wa mbolea au dawa za kuua vijidudu, hivyo unapaswa kuiosha sana kwa maji safi na kuiacha ndani ya maji safi kwa muda wa nusu saa kabla ya kuitumia ili kuua vijidudu hivi.

 

Angalizo:

Ulaji wa kabichi uliopitiliza huweza kusababisha ugonjwa wa rovu (goiter). kwahiyo watu wenye tatizo la rovu wasile kabichi kwa wingi.


Category: HEALTH | Added by: Admin (29/May/2013)
Views: 5672 | Tags: kabichi, faida, manufaa, afya, vitamin, saratani | Rating: 1.6/11
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: