Home » Articles » HEALTH

NJIA ZA KUTUMIA ILI UACHE KUVUTA SIGARA

NJIA ZA KUTUMIA ILI UACHE KUVUTA SIGARA


Tumeangalia madhara ya uvutaji wa sigara katika makala iliyopita, hebu tuangalie sasa ni njia zipi ambazo mtu anaweza kuzitumia ili aweze kuacha sigara. Lakini jambo la kufata kwanza kabla ya kufuata njia hizi ni kwamba uwe na nia hasa ya kuacha, Lakini kinyume na hapo hutaweza kufuata hatua hizi.

1.    Jambo la muhimu ni kwamba, uwe unahakika kabisa kwamba unataka kuacha kuvuta na kikubwa zaidi ili uepukane na madhara yake.

2.    Moja ya msaada bora wa kuacha kuvuta kunaweza kupatikana kwa kufanya mazoezi ya viungo. Hii ni tabia kama ile ya uvutaji wa sigara kwani kama nicotine inaongeza uchocheaji wa beta – endorphin, acetylcholine na adrenalin. Hivyo matokeo mazuri ya mazoezi haya ya viungo pia huchochea na kuleta hali ya pozo katika mwili, Lakini nicotine ina madhara.

3.    Tafuta siku maalum ya kuacha kuvuta sigara kama vile siku ya kuzaliwa, sherehe. Kisaikolojia unaweza kujikuta ukiacha kuvuta hata siku nyinginezo.

4.    Jitahidi uwe na nguvu ya hiari au nidhamu binafsi, hii itakusaidia pale utakapopata hamu ya kuvuta basi nguvu hii itakusaidia kupingana na hamu hiyo.

5.    Zidisha kula vyakula ambavyo haviendani kabisa na sigara kama vile, maziwa, juisi ya matunda badala ya chai na kahawa.

6.    Usipange kuvuta sigara, jitahidi uwe na ufahamu, ufahamu huu utakusaidia kuacha kuvuta kwani wanaovuta huwa hali hiyo inawatokea bila ya wao kufahamu kwani imekuwa ni kama sehemu ya maisha yao.

7.    Epuka kuchukua sigara au kukaa karibu na sigara kwani itakufanya upate hamu ya kuvuta tena pale utakapoiona hata kama una nia ya kuacha.

8.    Pale utakapohisi unapata hamu ya kuvuta, jitahidi utafute kazi nyingine haraka sana ili nafsi yako isikuzidi nguvu, tafuta kama kitu cha kula ili mdomo usiwe mtupu, au tafuta shughuli nyingine yoyote ambayo haiwezi kufanyika ukiwa unavuta.

9.    Epuka kukaa sehemu ambazo uvutaji wa sigara unafanyika sana, tafuta sehemu ambazo hakuna uvutaji wa sigara au uvutaji wa sigara uliopigwa marufuku.

10. Fanya sana mazoezi ya akili kama vile Meditation ili uifunze akili kuwa katika hali ya amani na utulivu pale unapopata hamu ya kitu ambacho kinaharibu mwenendo wa maisha yako, na pia mazoezi ya viungo ni muhimu sana kwani muda wa kuvuta sigara hautopatikana.

11. Jambo zuri jingine ni kwamba, kila utakapopata hamu ya kununua sigara chukua fedha hiyo na uihifadhi sehemu maalum. Fanya hivyo kwa muda wa mwezi kisha zichukue na uzihesabu, hapo utapata hamu ya kuacha sigara kisaikolojia kwa fedha hizo na kuona jinsi gani ulivyokuwa ukizipoteza.

Kwa upande wangu jaribu kufuata hizo hatua kumi huenda zikakusaidia sana katika kuacha kuvuta, Lakini hebu tuangalie taarifa ifuatayo ambayo imefanyiwa utafiti:

  1. Moja kati ya vifo vitatu vya saratani ni kutokana na uvutaji wa sigara.
  2. Moja kati ya vifo vitano vya matatizo ya moyo ni kutokana na uvutaji wa sigara.
  3. Tisa kati ya vifo kumi vya matatizo ya koo na kuharibika kwa mapafu ni kutokana na uvutaji wa sigara.
  4. Wastani wa mvutaji wa sigara hupungukiwa miaka nane ya muda wake wa kuishi kuliko asiyevuta na pia ana asilimia nusu tu ya kufikisha miaka 70 kuliko yule asiyevuta. Ingawa kifo hupangwa na Mungu, Lakini kila kifo kina sababu na huenda hii ikawa ndiyo sababu.
  5. Wavutaji huwa na asilimia sabini (70%) ya kiasi cha vifo (Death rate) kuliko wasiovuta.
  6. Uwezekano wa kupata matatizo ya moyo kwa wavutaji huwa mara mbili zaidi ya wasiovuta.
  7. Vifo vya ghafla hasahasa kwa vijana huwa mara nne kwa wavutaji kuliko wasiovuta na vilevile vifo vya wanaume  walio baina ya umri wa miaka 40 – 54 ni mara tatu kwa wavutaji kuliko wasiovuta.

Kwa upande wangu nina hayo tu, ikiwa una la kuongezea itakuwa ni vizuri sana kwani ndiyo wasaa mzuri wa kuelimishana na kutakiana mambo mazuri na yenye kuleta furaha katika maisha yetu. Kwa mawasiliano, maoni, ushauri na maswali,  jisikie huru kutuandikia. Tupo pamoja katika kuelimisha jamii na kutakiana kheri.

 

Category: HEALTH | Added by: Admin (19/Jul/2013) | Author: Yahyou M. Yahya E W
Views: 1342 | Rating: 0.0/0
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: